Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Mikoa wabadilishna uzoefu namna ya kuboresha huduma .

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili changamoto mbali mbali ambazo wataalamu wanakutana nazo wanapoleta wagonjwa wa hospitali ya (Upanga na Mloganzila) na namna watakavyoweza kuzitatua. Kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila na kushoto Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Rashid Mfaume.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na wataalamu kutoka Hospitali za Mikoa za Rufaa za Temeke, Mwananyamala, Amana na Tumbi walipokutana kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma za afya.

Baadhi ya wataalamu kutoka Muhimbili, Temeke, Mwananyamala, Amana, na Tumbi walio hudhuria kikao hicho.

Mkuu wa Idara ya Magojwa ya Ndani MNH-Mloganzila Dkt. Mwanaada Kilima akielezea baadhi ya huduma bobezi zinazotolewa katika hospitali ya Mloganzila.

Muuguzi Mkuu kutoka Hospitali ya Mwananyamala Bw. Musa Wambura akichangia mada wakati wa kikao hicho.

Mkuu wa Idara ya Mifupa na Ajali Dkt. Magdalena Mbeyale akielezea huduma zinazotolewa katika idara ya mifupa na ajali hospitali ya Mloganzila.


Na Priscus Silayo

Wataalamu wa Afya kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa washauriwa kujengeana uwezo na kupeana maarifa  kuhusu mbinu mbalimbali za kitabibu ili kuboresha matibabu kwa wananchi katika mikoa yao na kupunguza msongamano wa wagonjwa  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume wakati wa kikao baina ya wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na wataalamu kutoka Hospitali za Mikoa za Rufaa za Temeke, Mwananyamala, Amana na Tumbi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utoaji wa huduma za afya.

“Kikao hiki kitajadili changamoto ambazo wataalamu wa Hospitali za Rufaa za Mikoa wanakutana nazo pindi wanapoleta wagonjwa hospitali ya Muhimbili na pia tutaangalia changamoto ambazo wataalamu wa Muhimbili wanakutana nazo wanapowapokea wagonjwa hao, lengo kuu ni kutafuta namna ya kutatua changamoto hizo kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dkt. Mfaume 

Aidha Dkt. Mfaume aliitaka Hospitali ya Taifa Muhimbili kuendelea kuwalea wataalamu wa hospitali za mikoa kupitia majukwaa mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof.  Lawrence Museru amesema kuwa kupitia kikao hicho wataalamu wataweza kuunda mtandao (forum) ambao utamuwezesha daktari kutoka mahali popote alipo kuomba msaada kutoka kwa madaktari wengine wenye uzoefu au maarifa zaidi na hivyo kuondoa usumbufu wa kumsafirisha mgonjwa kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila)

Aidha Prof. Museru alibainisha kwamba kikao hicho kimefanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila ili kutoa fursa kwa wataalamu kutoka Hospitali za Mikoa za Rufaa kujionea huduma mbalimbali za kibingwa zinazotolewa Hospitalini hapo lakini pia uwekezaji mkubwa ambao serikali imeufanya.

“Tangu tulipokabidhiwa hospitali hii tumekuwa tukitafuta nafasi ya kukutana na waganga wakuu kutoka hospitali zenu, leo hatimaye tumekutana na ninaamini baada ya kikao hiki tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu na kuboresha huduma zaidi” Amesema Prof. Museru.

Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani MNH-Mloganzila  Dkt. Mwanaada Kilima amesema Mloganzila inatoa huduma za kibingwa na bobezi kwa kutumia vifaa vya kisasa vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu ambapo hospitali inafanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, mapafu, kifua sugu na magonjwa ya mfumo wa chakula.

Dkt. Mwanaada ameongeza kuwa kuna mashine za kisasa za CT Scan ambazo zinaweza kuchukua picha zote ikiwemo kichwa na moyo. Pia kuna vifaa na wataalamu wa kutosha wa fiziotherapia na  mazoezi tiba.