MNH yapokea vifaa tiba kusaidia watoto wenye saratani

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Rehema Laiti (kushoto) na Mkuu wa Jengo la Watoto, Bi. Mariana Makanda akipokea msaada wa vifaa tiba kutoka kwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bw. Silvian Sariko. Msaada huu umetolewa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya Saratani.

Wageni kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wakiwa na watoto wenye magonjwa ya saratani katika chumba cha kuchezea.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba nyenye thamani ya Tsh. 8,000,000 kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye magonjwa ya saratani.

Msaada huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Bw. Silvian Sariko kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa kituo ili kuwasaidia watoto hao.

Bw. Sariko amesema fedha za msaada huo zimetokana na fedha za wafanyakazi ambazo walilipwa baada ya kufanya kazi saa ziada.

“Kwa kauli moja tulikubaliana fedha hizi tuzitumie kununua vifaa tiba kwa ajili ya watoto hao badala ya kuzitumia kwenye matumizi mengine,” amesema Bw. Sariko.

Baada ya wageni hao kutembelea maeneo mbalimbali katika wodi ya watoto hao, wameahidi kuendelea kwasaidia zaidi hasa katika maeneo ya kucheza, kusomea na wodini. 

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Rehema Laiti ameshukuru LHRC kutoa msaada huo kwani utasaidia kurahisisha matibabu yao.

Amesema watoto wenye saratani wanachukua miezi sita hadi miaka mitatu kupata matibabu sambamba kufutilia matibabu baada ya kuruhusiwa.