Mloganzila yapokea msaada wa kujikinga na COVID-19

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi (kushoto) akipokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka kwa mwakilishi wa Taasisi ya Helping Hands Tanzania Bi. Fadhiya Khatib

Dkt. Magandi na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MNH-Mloganzila Sr. Redemptha Matindi wakionyesha nguo ya kujikinga (PPE) lililokabidhiwa hospitalini hapa leo.


Na Lightness Mndeme

Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila imepokea msaada wenye thamani ya TZS. 9milioni wa vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona, kutoka kwa taasisi isiyo ya kiserikali ya Helping Hands Tanzania.

 
Msaada huo umejumuisha mipira ya kuvaa mikononi (gloves) boksi 100, barakoa 1300 (1250 barakoa za upasuaji na 50 ni za N95), Aproni za kutumia bila kurudia 500 (disposable), nguo za kujikinga (PPE) 5, mabuti 10, jiki lita 100, vitakasa mikono chupa 6, chupa 6 za detol ya maji na vifaa vya kujikinga uso 10.


Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa msaada ambao utasaidia kuwakinga watoa huduma hospitalini hapa.


“Tunawashukuru sana kwa msaada huu ambao umekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu ikipambana na ugonjwa wa Covid-19 vifaa hivi vitasaidia kuwakinga watoa huduma wetu walioko mstari wa mbele kuhudumia watu mbalimbali wanaofika hospitalini hapa” amesema Dkt. Magandi.


Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mwakilishi kutoka Helping Hands Tanzania Bi. Zubeda Ramzan amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.


“Tumeamua kutoa msaada huu ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 jamii ielewe kuwa bila watumishi wa afya vita hii hatutashinda hivyo tuungane kwa pamoja katika mapambano haya na hakika tutashinda” amesema Bi. Ramzan.

Bi. Ramzan ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia watoa huduma kwa kuwapatia vifaa vitakavyosaidia kuwakinga pindi wanapotoa huduma.