Mloganzila yapokea msaada wa darubini ya upasuaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru (katikati) akizungumza wakati wa kupokea msaada wa mashine ya kufanyia upasuaji wa macho (Operating Microscope), kushoto ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi, kulia ni Bi. Jihye Kim akifuatiwa na Shukuru Mtenga kutoka Taasisi ya Vision Care.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care Bi. Jihye Kim akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo ili kupambana na magonjwa ya macho na kuzuia upofu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila, Catherine Makunja akielezea umuhimu wa mashine na namna itakavyoweza kuleta manufaa kwa kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapa.

Prof. Museru na Dkt. Magandi pamoja Dkt. Makunja wakipokea sehemu ya mashine ya kufanyia upasuaji wa macho (Operating Microscope) kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care Bi. Jihye Kim.

Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya vingozi wa MNH-Mloganzila na wawakilishi kutoka Vision Care baada ya kukabidhiwa msaada huo.


Na Dorcas David

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa mashine ya upasuaji wa macho (Operating Microscope) yenye thamani ya takribani TZS. 41 Mil. kutoka Taasisi ya Vision Care inayojihusisha na mapambano dhidi ya matizo ya upofu duniani.

Msaada huo unalenga kuisaidia hospitali katika kuendelea kutoa huduma bora na za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo ya macho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru ameishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za hospitali katika kuboresha huduma.

“Msaada huu umekuja wakati muafaka na tunauhitaji mashine kama hii ambayo itatusaidia kuongeza tija katika huduma zetu hasa katika Idara ya Magonjwa ya Macho, tunawashukuru sana  kwa ushirikiano wenu katika kuboresha huduma za afya,”amesema Prof. Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila, Catherine Makunja amesema mashine ya upasuaji wa macho (Operating Microscope) ni muhimu kwani kila mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji wa jicho lazima atapaswa kuitumia mashine hiyo.

“Jicho ni kiungo kidogo ambacho upasuaji wake unahitaji umakini wa hali ya juu na Operating Microscope ndio mashine pekee ambayo itamsaidia daktari kufanya upasuaji,”amesema Dkt. Makunja.

Kwa mujibu wa Dkt. Makunja tatizo la macho limeongezeka kwa sasa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha ambapo katika Kliniki ya Magonjwa ya Macho Mloganzila, wagonjwa 350 hadi 400 huonwa kwa mwezi na baadhi yao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care, Bi. Jihye Kim amesema wanayofuraha kukabidhi msaada huu ambao utasaidia wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi na kuahidi kuendeleza mahusiano.