Miaka minne ya JPM, Muhimbili yatekeleza maagizo yake kikamilifu

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu mafanikio ya MNH katika kipindi cha miaka minne ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imefanikiwa kutekeleza maagizo saba ya Rais John Pombe Magufuli likiwamo la upatikanaji wa dawa kwa asilimia 96 na kutoa huduma za ubobezi ili kupunguza rufaa nje ya nchi, wagonjwa waliokuwa wakilala chini kupatiwa vitanda, kulipa stahiki za wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi, kununua na kukarabati vitendea kazi na kuondoa kero ya MRI na CT-scan.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maagizo haya miaka minne iliyopita baada ya kuingia madarakani mwaka 2015, lengo kubwa likiwa ni kuboresha huduma za matibabu katika hospitali ya Muhimbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru kuhusu mafanikio ya MNH katika kipindi cha miaka minne ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, amesema katika uwekezaji ambao ulilenga kutekeleza maagizo ya Rais, hospitali ilitumia shilingi bilioni 37.4 kununua vifaa tiba na mashine, kuboresha miundombinu na kujenga uwezo wa wataalamu.

Prof. Museru amesema kuwa MNH, iliokoa jumla ya shilingi bilioni 32 kwa kutoa huduma ya upandikizaji figo kwa wagonjwa 51 tangu kuanzishwa kwa huduma hii Novemba 2017, upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia kwa wagonjwa 34, huduma ya magonjwa ya  mfumo wa chakula na Ini imetolewa kwa wagonjwa 380 na kutoa huduma ya tiba radiolojia kwa wagonjwa 558 tangu kuanza kwa tiba hii Novemba 2017.
 
Mkurugenzi Mtendaji amefafanua kwamba katika kipindi cha miaka minne, hospitali imetumia Shiligi bilioni 72 bilioni kununua dawa na kusaidia wagonjwa kupata dawa kwa asilimia 96 tofauti na awali dawa zilikuwa zikipatikana kwa asilimia 40.

Pia, amesema wagonjwa walikuwa wakilala chini hivi sasa wamepatiwa vitanda na kwamba hivi sasa tatizo hilo limekwisha kufuatia kuhama kwa wagonjwa wa Taasisi ya Mifupa (MOI) kutoka wodi za Muhimbili walizokuwa wakitumia ambazo ni wodi 17, na 18 zilizoko jengo la Sewahaji na wodi namba mbili iliyoko jengo la Mwaisela ambayo hivi sasa ni ICU yenye vitanda 15.
Prof. Museru amesema katika kipindi cha miaka minne, hospitali imelipa wafanyakazi malimbikizo ya madai yao ambayo walikuwa wakidai kwa kipindi kirefu kama malipo ya on call, malipo ya wauguzi ya usiku, malipo ya posho mbalimbali hasa kwa madaktari pamoja na kada nyingine za afya.

“Kutolipwa kwa wafanyakazi, hali hii ilishusha morali kwa kiwango kikubwa sana na hivyo wafanyakazi kupunguza kasi ya ufanyaji kazi na hivyo tija kukosekana. Kwa sasa wafanyakazi wengi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wana hari ya kufanya kazi,” amefafanua Prof. Museru.

Katika mkutano huo, Prof. Museru amewaeleza waandishi kwamba  kwa nyakati tofauti hospitali ilipeleka wataalamu wa aina mbalimbali nje ya nchi kwa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu wakiwemo madaktari bingwa, wauguzi, wataalamu wa maabara, wataalamu wa radiolojia, watalaamu wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, watalaam wa saratani za damu ili kupata ujuzi na elimu ya kutoa huduma hizi kwa ufanisi.
 “Mafunzo haya yamegharimu Muhimbili  shilingi Bilioni 3.597  na hivyo Watanzania wengi kuhudumiwa hapa nchini badala ya kupelekwa nje na pia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali za umma,” amesema Prof. Museru.
Katika hatua nyingine, Prof. Museru amesema tangu Oktoba 3, 2018, MNH ilipokabidhiwa kusimamia Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, imefanikiwa  kufanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe katika mishipa ya damu kwenye ubongo  ambapo gharama za upasuaji kwa mgonjwa mmoja ni Shilingi milioni 20 na nje ya nchi ingegharimu shilingi milioni 40 na kwamba wagonjwa wanne wamegharimu shilingi milioni 80 badala ya shilingi milioni 160 endapo wangetibiwa nje ya nchi na kuokoa shilingi milioni 80.

Pia, amesema Hospitali ya Muhimbili- Mloganzila imefanya upasuaji wa matatizo ya mgongo (Spinal surgery) na hivyo imekua hospitali ya pili ya umma nchini kwa kutoa huduma hii baada ya MOI.

“Tangu kufunguliwa kwa Hospitali hii ya Mloganzila wagonjwa 869 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wamepokelewa hospitalini hapa na kupatiwa huduma, hatua ambayo imepunguza msongamano wa wagonjwa Muhimbili,” amesema Prof. Museru.

Akizungumzia mipango ya baadaye, Prof. Museru amesema hospitali inakusudia kujenga jengo la ghorofa tatu kwa ajili ya wagonjwa wa kulipia au wagonjwa binafsi (IPPM) litakalokuwa na vyumba 20 vya kulala mgonjwa mmoja mmoja, vyumba 20 vya kulala wagonjwa wawili wawili, vyumba vitano vya kulaza watu mashuhuri (VIP) na chumba kimoja cha kulaza iiongozi wa kitaifa (Presidential suite).