Kumi kufanyiwa upasuaji wa kuondolewa mafindofindo Ligula

Daktari Bingwa wa upasuaji pua, koo na masikio Willybroad Massawe akimtoa mgonjwa matezi ya koo na matezi ya nyama ya pua (mafindofindo), upasuaji huo umefanyika leo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mtwara-Ligula-.

Mtaalam wa usingizi (nusu kaputi) Dkt. Amon Kingu (kushoto) pamoja na watalaam wengine wa Hospitali ya Ligula wakiwamuandaa mgonjwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.


Na Neema Wilson Mwangomo

Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mtwara-Ligula- leo wanawafanyia upasuaji wagonjwa 10 wenye matatizo ya mafindofindo.
Matibabu hayo ya kibingwa hayafanyiki katika Hospitali ya Ligula kutokana na ukosefu wa wataalam waliobobea katika maeneo ya pua, koo na masikio.
Daktari Bingwa wa upasuaji pua, koo na masiko kutoka Muhimbili Willybroad Massawe amesema wanawafanyia upasuaji watu wazima pamoja na watoto na kwamba upasuaji huo umeanza kufanyika leo.
‘’Tumeanza kufanya upasuaji huu leo asubuhi na lengo letu ni kumaliza wagonjwa wote kumi leo hii’’ amesema Dkt. Massawe.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo ugonjwa wa mafindofindo unasababishwa na maambukizi ya mara kwa mara katika njia ya hewa na kwa wengine unatokana na mzio (allergies) zilizokithiri.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeanzisha programu ya kutoa huduma kwa njia ya mkoba ili kujenga uwezo wa Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini hasa katika maeneo yenye wataalam lakini wanahitaji kuongezewa ujuzi zaidi katika fani mbalimbali ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa Muhimbili.