KOFIH kuendeleza ushiriakino na Mloganzila

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (kulia) akimsikiliza Naibu Balozi wa Korea Tanzania Bi. Heashin Anh (katika), kushoto ni Bi. Jungyoon Kim.

Dkt. Juelieth Magandi akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Balozi wa Korea Tanzania walipotembelea Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kukagua miradi wanayofadhili.

Muuguzi Mwandamizi chumba cha upasuaji Sis. Kanaeli Uriyo akielezea moja ya mashine zilizopo katika Idara ya Upasuaji (Endoscopic Towers) ambazo hazitumiki kutokana na ukosefu wa baadhi ya vifaa.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (katikati) na baadhi ya viongozi wa Mloganzila wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Balozi wa Korea Tanzania aliyeambatana na mwakilishi kutoka Taasisi ya Korea Foundation For International Healthcare (KOFIH).


Na Dorcas David

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeshukuru Serikali ya Korea kupitia Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) ambayo inamchango mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya ikiwemo za ubingwa wa juu.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Naibu Balozi wa Korea Tanzania aliyeambatana na mwakilishi wa Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) ambao wametembelea Hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kukagua miradi wanayofadhili ili kuboresha zaidi.

Dkt. Magandi ameeleza kwamba KOFIH imekua mstari wa mbele kusaidia hospitali katika maeneo mbalimbali ambapo katika kipindi cha Juni mwaka huu African Future Foundation kupitia KOFIH walielekeza wataalamu namna yakutumia  mashine ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko (Extracorporeal shock wave lithotripsy -ESWL) na kufanikiwa kuanza kutoa huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa njia ya kisasa ambapo mpaka sasa jumla ya wagonjwa 60 wamenufaika na huduma hiyo .

 “Tunawashukuru KOFIH, ushirikiano huu umesaidia kuongeza tija katika utoaji wa huduma za kibingwa kwani umewezesha Hospitali ya Mloganzila kutoa huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa njia ya kisasa, pia mwezi wa nane mwaka huu tulipokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS. 331,383,000 Mil ambao ulilenga kuisaidia hospitali kuendelea kutoa huduma bora na za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wanaofika kupatiwa matibabu hospitalini hapa” amesema Dkt. Magandi.

“Msaada huo ulijumuisha vifaa tiba vya kufanyia upasuaji masikio, pua na koo na vifaa vya ufundi kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba’’ amefafanua Dkt. Magandi.

Kwa upande wake Naibu Balozi wa Korea Tanzani Bi. Heashin Ahn amesema wataendelea kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa karibu katika kuhakikisha wataalamu wanapatiwa mafunzo na vifaa tiba vitakavyowasaidia kutimiza majukumu yao ya kila siku.
 
Mwishoni mwa mwaka jana Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) ilitoa mafunzo ya mwezi mmoja kwa  wataalamu wa vifaa tiba kutoka Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Lindi, Tanga, Geita, Mwanza, Arusha, Pwani, Mtwara, Singida, Mbeya, Kilimanjaro, Shinyanga na Katavi.