Katibu Mkuu Aiagiza Muhimbili Kutoa Huduma za Afya nje ya Nchi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika mkutano wa ufunguzi wa huduma ya afya kwa njia ya mkoba ambayo imeanza kutolewa leo na wataalamu wa afya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na watalaamu wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma.

Baadhi ya wataalamu wa Muhimbili wakimsikiliza Katibu Mkuu katika mkutano wa ufunguzi wa huduma ya afya kwa njia ya mkoba ambayo imeanza kutolewa leo katika Hospitali ya Rufaa ya Musoma.

Kutoka Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Carolina Mtapula, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Francis Mwanisi na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma, Dkt. Joachim Eyembe wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Ulisubisya.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Brighton Mushengezi akimsikiliza mmoja wa wagonjwa waliofika leo katika Hospitali ya Rufaa ya Musoma kupata huduma.

Katika picha ni baadhi ya wagonjwa waliofika leo Hospitali ya Rufaa ya Musoma kwa ajili ya kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu.

Mmoja wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa Musoma akipatiwa huduma na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Muhimbili, Dkt. Athumani Mbalamula.

Baadhi ya wagonjwa wenye matatizo ya macho wakimsiliza mtaamu wa hospitali hiyo leo.

Daktari Bingwa wa Kinamama, Dkt. Helen Mrina akimsikiliza mmoja wa wagonjwa aliyefika kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Ulisubisya akiwa katika picha ya pamoja leo na wataalamu wa Muhimbili na wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma.


Na John Stephen

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya ameagiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuendelea kutoa huduma za afya kwa njia ya mkoba katika hospitali za rufaa nchini na baadaye katika nchi za nje ya Tanzania.

 Kauli hiyo imetolewa leo mkoani Mara wakati Dkt. Ulisubisya akifungua huduma kwa njia ya mkoba ambayo imeanza kutolewa leo na watalaamu wabobezi wa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma.

Dkt. Ulisubisya amewataka watalaamu wabobezi wa Muhimbili kwenda katika hospitali nyingine za rufaa nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali hizo pamoja na kutoa huduma mbalimbali za afya ambazo zimeshindikana.

“Wataalamu wa Muhimbili wamekuja hapa Musoma kushirikiana na wataalamu wa hospitali hii kutoa huduma ambazo zimeshindikana hapa. Watatoa ujuzi wao ili kuwawezesha wataalamu wa Musoma kutoa huduma bora zaidi,” amesema Dkt. Ulisubisya.

Dkt. Ulisubisya amewataka kwenda nje ya nchi kwa ajili kutoa huduma za afya na kubadilishana uzoefu na kwa kuanzia amewataka kuanza kutoa huduma za afya nchini Comoro.

Akiwa katika hospitali hiyo ya rufaa, Dkt. Ulisubisya amewapongeza wataalamu wa Muhimbili kwa kufika Musoma kwa ajili ya kutoa huduma hiyo huku akiwataka wataalamu wa Hospitali ya Rufaa Musoma kwenda katika hospitali za wilaya kutoa ujuzi ambao watakuwa wameupata kutoka kwa wenzao wa Muhimbili.

Katibu huyo amewataka viongozi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujisajili katika taasisi husika na kupatiwa vitambulisho vya bima ya afya.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joachim Eyembe mbali ya kuishukuru Muhimbili pamoja na serikali kutokana na juhudi zake za kuendelea kutoa huduma bora nchini, amesema hospitali yake ina watumishi 306 na kwamba ina upungufu wa watumishi 375 sawa na upungufu wa asilimia 55.1.

Pia, amesema hospitali hiyo imefanikiwa kufungua duka la dawa la hospitali, kuanzisha huduma za kibingwa kwa kutumia madaktari kutoka Hospitali ya Bugando na kununua komyuta 40.

Katika hatua nyingine, Mkazi wa Mkoa wa Mara, Easter Juma amesema wamekuwa na matatizo ya siku nyingi hivyo wameiomba serikali ipeleke wataalamu bingwa katika hospitali hiyo kila baada ya miezi minne.

Naye Yusuph Abdallah Chamba ambaye ni mkazi wa Musoma amesema wamafurahi kupatiwa huduma za kibingwa na kwamba wameiomba serikali kufanya mpango huo kuwa wa mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi wa mkoa huo. Pia ameiomba serikali kuongeza wataalamu zaidi kwani hivi sasa hospitali hiyo ina upungufu wa madaktari.

Tayari watalaamu wa Muhimbili kwa kushirikiana na wa Hospitali ya Rufaa Musoma wameanza kutoa huduma kwa watu mbalimbali waliojitokeza kwa wingi wakiwamo wanafunzi, kinamama na wazee.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)