Jamii yatakiwa kupima macho kuzuia upofu, uoni hafifu

Afisa Muuguzi wa macho, Bw. Sebastian Luzinga akimfanyia uchunguzi wa awali kwa kumtaka kusoma maandishi maalumu ya kutathmini uono wa mteja aliyefika Banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili lililopo viwanja vya Sabasaba.

Wananchi mbalimbali wakizingatia maelekezo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kunawa mikono na maji tiririka na kutumia vitakasa mikono kabla ya kuingia kwenye Banda la Muhimbili lililopo viwanja vya Sabasaba.

Wananchi mbalimbali wakiingia na kutoka kwenye Banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila kupata huduma mbalimbali zinazopatikana katika banda hilo.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto, Dkt. Deogratious Mally akitoa elimu ya jinsi ya kuhudumia watoto wanaohitaji uangalizi maalumu.

Mtaalamu kutoka Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Bi. Hadija Thabiti akimpatia barakoa na kumuelekeza matumizi sahihi mwananchi aliyefika Banda la Muhimbili kupata huduma.

Mwananchi aliyefika Banda la Muhimbili akipima uzito kabla ya kuanza kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Alphonce Simbila akiwaelimisha watoto namna mgonjwa wa dharura na ajali anavyohudumiwa anapofikishwa Hospitali ya Muhimbili.

Daktari wa Magonjwa ya Macho, Yusta Mtogo akimfanyia uchunguzi wa macho mtoto Mary Christopher aliyeletwa katika Banda la Muhimbili.


Na John Stephen

Jamii imetakiwa kujenga mazoea ya kupima afya ili kuzuia magonjwa ya macho kama vile, shinikizo la jicho, uono hafifu na wakati mwingine upofu.

Wataalamu wa afya wameshauri jamii kupima macho kwa sababu watu wengi wana matatizo makubwa ya macho kutokana na kuchelewa kwenda hospitali.

Mtaalamu wa macho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Neema Moshi amesema magonjwa ya macho yapo ambayo yanaonyesha dalili na mengine hayaonyeshi katika hatua za awali.

“Yapo magonjwa ya macho yanayokuja na uvimbe, maambukizi na wakati mwingine mtu anapoteza uono kwa haraka, lakini magonjwa ya macho mengine hayana dalili katika hatua za awali kama shinikizo la jicho na uharibifu wa jicho kutokana na magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, seli mundu na UKIMWI” amefafanua Dkt. Neema.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Yusta Mtogo wa Hospitali ya Taifa-Mloganzila ameitaka jamii kupima afya mara kwa mara kwa kuwa magonjwa mengi ya macho yanasababisha upofu unaozuilika.   

Akizungumzia suala la baadhi ya watu kufikiri kwamba kuvaa miwani wataonekana wazee au kusababisha uharibifu wa macho, Dkt. Mtogo amesema si kweli na kwamba wanaovaa miwani ni tiba kama tiba nyingine.

“Watoto kutokuvaa miwani baada ya wataalamu wa macho kubaini ana magonjwa ya macho kunaweza kusababisha uono hafifu, hivyo basi miwani ni muhimu kwa watoto,” amesema Dkt. Mtogo.