Jamii yatakiwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku

Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga, Dkt. Christopher Rweihimba akimfanyia uchunguzi wa afya ya kinywa na meno mmoja wa wananchi waliotembelea Banda la Muhimbili liliopo Viwanja vya Sabasaba kupata huduma kupata huduma.

Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga, Bi. Zuhura Mawona (kushoto) pamoja na wananchi wakipata maelezo namna ya kumhudumia mgonjwa wa dharura na ajali kutoka kwa Afisa Muuguzi wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Bw. Chimpaye Yusuph.

Daktari wa Magonjwa ya Dharura kutoka MNH-Mloganzila, Dkt. Gerald Kalinga akitoa elimu kwa wananchi namna ya kumhudumia mgonjwa wa dharura na ajali.

Wananchi mbalimbali wakipata elimu ya namna ya kumhudumia mtoto anayehitaji unagalizi maalumu.


Na Priscus Silayo

Jamii yashauriwa kupiga mswaki kwa ufanisi-mara mbili kwa siku ili kujikinga na maradhi ya kinywa na meno.

Wananchi wametakiwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku asubuhi kabla ya kifungua kinywa asubuhi na jioni baada ya chakula kabla ya kulala.

Hayo yamesemwa na Daktari wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga, Dkt.  Christopher Rweihimba wakati akitoa elimu ya kukabiliana na magonjwa ya afya kinywa na meno katika Maonyesho ya 45 ya Sabasaba.

Dkt. Rweihimba amesema midomo yetu imejaa bakteria na vimelea hawa pamoja na mabaki ya chakula ambayo huunda tabaka kwenye kuta za meno na fizi.

Amesema kutokana na kuwapo kwa bakteria kwenye kinywa, jamii inapaswa kupiga mswaki kwa ufanisi na kutumia Kamba (floss) ili kusaidia kuondoa tabaka hili.

“Tabaka hili lisipoondolewa hukomaa na kuwa tabaka gumu liitwalo ugaga (calculus) ambalo halisafishiki mpaka mtu afike hospitalini kwa mtaalamu wa kinywa na meno.

 Pia, ameeleza sababu nyingine zinazosababisha magonjwa ya afya ya kinywa na meno ni pamoja na uvutaji wa sigara, matumizi ya baadhi ya dawa, maradhi yanayosababisha kushuka kwa kinga za mwili mfano kisukari.

Dkt. Rweihimba amesema, kwa wagonjwa waliofika kupata huduma za kiuchunguzi katika banda la idara ya kinywa na meno Sabasaba, maradhi ya fizi ndiyo yamekuwa kinala ambapo kati ya wagonjwa waliofika kwa wataalamu, asilimia 65 wamebainika kuwa na tatizo la maradhi ya fizi.

Amefafanua kwamba mtu mwenye maradhi ya fizi ana harufu mbaya mdomoni, lakini hajitambui kama kinywa chake kinatoa harufu.

Amesema dalili nyingine za maradhi ya fizi ni fizi kuvimba, kuwa mwekundu na kutoa damu, mtu kuwa na utando wa ugaga unaozunguka meno na fizi, meno kulegea, kuwa na maumivu na hatimaye kutoka.

“Ili kujikinga na maradhi ya afya kinywa na meno, jamii inapaswa kusafisha meno kwa kutumia Kamba maalumu (floss) angalau mara moja kwa wiki, kutumia dawa ya meno yenye madini ya floraidi kama ilivyoelekezwa na wataalamu wa afya ya kinywa na meno,” amefafanua Dkt.Rweihimba.

Magonjwa ya afya ya kinywa na meno yanatibika endapo mtu atazingatia usafi wa kinywa na meno, kufika hospitalini mapema baada ya kuona atakapoona dalili za magonjwa ya afya ya meno.