‘Jamii jitokezeni kuchangia damu kuokoa maisha ya wagonjwa’

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Praxeda Ogweyo akizungumza na waandishi wa Habari katika maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu duniani ambayo hufanyika Juni 14, kila mwaka. Kushoto ni Msimamizi wa Jengo la Maabara Kuu, Bi. Grace Lugemwa na kulia ni Dkt. Mabula Kasubi, Mkuu wa Idara ya Pathologia hospitalini hapa.

Wachangiaji damu wakiwa katika maadhimisho hayo.

Baadhi ya wananchi wakichangia damu ikiwa sehemu ya kushiriki katika maadhimisho hayo.

Mmoja wa wachangiaji damu, Bw. Donald Francis akipokea cheti kutokana na ushiriki wake mara kwa mara. Bw. Donald amechangia damu mara 66 tangu mwaka 1992.

Dkt. Ogweyo akimkabidhi cheti Bw. Hassan Mohamed Kiweko kutokana ushiriki wake wa mara kwa mara.

Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama hospitalini hapa, Dkt. Neema Lubuva akizungumza na vyombo vya Habari.

Kushoto ni Dkt. Mabula Kasubi, Mkuu wa Idara ya Pathologia hospitalini hapa akiwa na Mratibu wa Uchangiaji Damu Muhimbili, Bw. John Bigambalaye.

Baadhi ya watumishi wa Muhimbili wakiwa katika picha ya pamoja na wachangia damu.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imeomba jamii kujitokeza mara kwa mara kuchagia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wa saratani za damu, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, wanaopata ajali, kina mama wajawazito na watu wengine wenye uhitaji wa damu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili katika maadhimisho ya uchangiaji damu duniani ambayo huadhimishwa Juni 14, kila mwaka, Dkt. Praxeda Ogweyo amesema mahitaji ya damu ni makubwa hivyo watu mbalimbali wakiwamo ndugu wa wagonjwa na wafanyakazi katika taasisi mbalimbali wanapaswa kujitokeza ili kuokoa maisha ya makundi hayo.

Mbali na hayo mabalozi wanaochangia damu mara kwa mara kwenye hospitali hiyo, pia walijitokeza na kujumuika na watu mbalimbali katika maadhimisho hayo

Dkt. Ogweyo amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kuchangia damu kwa kuwa uhitaji wa damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni chupa 100 hadi 120 kwa siku na kwamba kiwango cha ukusanyaji damu kwa siku ni chupa 70 hadi 100.

“Kwa takwimu hii, mahitaji ya damu bado ni makubwa, lakini kwa msaada na ushirikiano kutoka kwa wadau kama ninyi wachangiaji damu, tunaamini tutafanikiwa kuendelea kuokoa maisha ya kina mama wajawazito, wanaopata ajali, wagonjwa wa saratani za damu na wengine wenye uhitaji wa damu,” amesema Dkt. Ogweyo.