Dkt. Magandi: Wataalamu tarajali jengeni taswira nzuri kwa wananchi

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa madaktari na wauguzi tarajali kulia ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu na Utawala Bi. Njoikiki Mapunda.

Wataalamu tarajali wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo.

Mkuu wa Idara ya Uuguzi, Ubora na Mazingira wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Bi. Clauda Miombo akiwasilisha mada kuhusu huduma bora kwa wateja.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ufundi wa Hospitali ya Mloganzila, Mhandisi Veilla Matee akisisitiza matumizi bora na utunzaji wa vifaa tiba hospitalini hapa.


Na Dorcas David

Wataalamu tarajali wa kada za afya kutoka vyuo mbalimbali nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya kazi ili kuendelea kujenga taswira nzuri kwa wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo.

Kauli hiyo, imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku mbili kwa wataalamu hao kuhusu maadili ya utumishi wa umma mahala pa kazi.

Amesema uwajibikaji ni jambo muhimu katika kuboresha huduma za afya na kwamba uongozi hautakuwa tayari kumvumilia mtumishi asiyetaka kutimiza wajibu wake kama inavyotakiwa.

Dkt. Magandi amewataka wataalamu hao kuweka malengo ya kujifunza kwa bidii ili kupata ujuzi wa kutosha katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho watakuwepo katika hospitali hiyo.

Mkuu wa Idara ya Uuguzi, Ubora na Mazingira wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Bi. Clauda Miombo amesema wagonjwa wanapata matumaini pale wanapopokelewa kwa ukarimu na mahitaji yao kusikilizwa kwa wakati.

 “Mgonjwa ni balozi mzuri sana kwani ukimuhudumia vizuri basi atajenga taswira nzuri ya hospitali na wananchi watakuwa na imani kuhusu huduma zinazotolewa na wataalamu wetu,” amesema Bi. Miombo. 

Naye, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ufundi wa Hospitali ya Mloganzila, Bi. Veilla Matee amewasisitiza wataalamu hao kuhakikisha wanatumia vifaa kwa uangalifu ili vidumu kwa muda mrefu na kupunguza gharama za matengenezo.

Mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Mloganzila yamehusisha wataalamu tarajali 125 kutoka kada mbalimbali za afya.