Dkt. Gwajima: Nimefarijika Muhimbili inavyosimamia mchakato wa manunuzi katika hospitali tano

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na viongozi na wawakilishi wa hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), hospitali za rufaa; Temeke, Mwananyamala, Amana na Tumbi.

Baadhi ya viongozi na wawakilishi wa hospitali wakiwa kwenye kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na baadhi ya wawakilishi wa hospitali za rufaa nchini.

Baadhi ya wawakilishi wa hospitali za rufaa.


Na Angel Mndolwa

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema amefarijika jinsi  Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inavyosimamia mpango wa maendeleo wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 wenye thamani ya TZS. 25 bilioni.

Fedha hizo, zitatumika kununua vifaa tiba katika hospitali tano ikiwamo MNH, hospitali za rufaa; Temeke, Mwananyamala, Amana na Tumbi. 

Akizungumza katika kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya mapambano dhidi ya UVIKO-19 pamoja na mchakato wa manunuzi ya vifaa tiba, Dkt. Gwajima amesema maendeleo ya uuandaji wa manunuzi wa vifaa tiba katika hospitali hizo ni mazuri na kwamba mikataba ya ununuzi wa vifaa hivyo ipo mbioni kusainiwa.

“Mikataba ya ununuzi wa vifaa tiba uko mbioni kusainiwa na baada ya mwaka mpya, tutakuwa na vikao kila baada ya siku saba,” amesema Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima.

Pia, Waziri wa Afya. Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba wizara yake itakuwa ikifuatilia mara kwa mara maendeleo ya mpango huo kwa kutoa ripoti ya mradi huo inapaswa kufungwa Aprili, mwaka 2022.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amawataka viongozi na wawakilishi wa hospitali hizo kujadili na kutengeneza mfumo wa pamoja wa utoaji wa taarifa za matumizi ya fedha za mpango huo. 

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru amemuahidi Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima kwamba Muhimbili itaendelea kufuata taratibu za manunuzi ili kufanikisha kwa wakati mchakato wa ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya hospitali hizo.

 “Mheshimiwa Waziri, nakuhakikishia kwamba kila kitu kitakwenda vizuri,” amesema Prof. Museru.