DART & UDART watoa zawadi kwa wagonjwa Mloganzila.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza na baadhi ya viongozi wa DART na UDART mapema kabla ya viongozi hao kumkabidhi zawadi mbalimbali zilizotolewa na wanawake ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Dkt. Julieth Magandi akipokea zawadi kwaajili ya wagonjwa wanawake kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu DART, Dkt. Philemon Mzee zilizotolewa na wanawake wa DART na UDART kwa wagonjwa wanawake Mloganzila, katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Sis. Redemptha Matindi.

Dkt. Julieth Magandi na baadhi ya viongozi wa MNH-Mloganzila wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi kutoka DART na UDART waliokuja kutembelea wagonjwa na kutoa zawadi kwa wagonjwa wanawake.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Sis. Redempth Matindi akielezea namna zawadi hizo zitakavyotumika.

Baadhi ya watumishi kutoka DART na UDART wakichangia damu.


Na Priscus Silayo

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea zawadi mbalimbali zenye thamani ya TZS 1, 600, 000 kutoka kwa wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) na Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDART) ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8, kila mwaka.

Zawadi zilizotolewa ni mashuka, ndala za kuogea, sabuni za miche, sabuni za kuogea, sabuni ya unga, mafuta ya nazi kwa ajili ya watoto, mafuta ya kupaka. 

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amewashukuru DART na UDART kwa msaada huo kwani utasaidia kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.

“Kwa niaba ya uongozi wa Mloganzila napenda kutoa shukrani za dhati kwa wafanyakazi wanawake wa DART na UDART kwa msaada huu mlioutoa ambao tumeugawa kwa kina mama, muendelee na moyo huo huo wa upendo wa kuisadia jamii” amesema Dkt. Magandi

Dkt. Magandi ameongeza kuwa MNH-Mloganzila, DART na UDART wamekuwa na ushirikiano mzuri ambapo ushirikiano huo umesaidia kutatua changamoto ya usafiri kwa ndugu, wagonjwa pamoja na wafanyakazi wa hospitalini hapo kwa kuanzisha usafiri wa Mabasi yaendayo haraka kuelekea maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu DART, Dkt. Philemon Mzee amesema kwa kutambua umuhimu wa siku ya Wanawake Duniani, uongozi wa DART kwa kushirikiana na UDART umeona uwaunge mkono wanawake kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa wanawake hapa Mloganzila.

“Mtaona leo ni siku ya wanawake ila kama menejimenti tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuwasindikiza wakina mama kwa lengo la kuja kuwapa wakina mama wenzao zawadi mbalimbali,kuwajulia hali na kuwapa faraja pia” amesema Dkt. Mzee.

Katika hatua nyingine Dkt. Mzee ameongeza kuwa DART itaendelea kuboresha usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa kujenga eneo la kusubiria abiria hivi karibuni ili kuondoa adha wanayoipata husani nyakati za mvua na jua kali ambapo pia imekuwa malalamiko ya abiria.

Kwa upande wake Bi. Sofia Issa miongoni mwa wagonjwa waliopata msaada amewashukuru DART, UDART na uongozi Hospitali ya Mloganzila kwa huduma wanazozitoa kwa wagonjwa kwani zina ubora wa hali ya juu.

Pamoja na kutoa zawadi hizo, DART &UDART wametumia fursa hiyo kujitolea kuchangia damu ambapo jumla ya Unit 3 zimepatikana.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu kimkoa yamefanyika katika uwanja wa Uhuru, kauli mbiu ya mwaka huu ni “kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu, jitokeze kuhesabiwa”.