Dar es Salaam’s British Legion Tanganyika Club yapiga jeki kiwanda Muhimbili

Mwenyekiti wa Dar es salaam’S British Legion Tanganyika Club Bw. Godfrey Mramba (kushoto) akikabidhi msaada wa TZS. 5,425,000 Mil. kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru (kulia) ili kuongeza nguvu kwenye kiwanda cha kuzalisha mavazi kinga ya kujikinga na maambukizi ya Covid-19.

Bw. Godfrey Mramba na Prof. Lawrence Museru wakiangalia Barakoa zilizoanza kuzalishwa Muhimbili ambazo zitatumiwa na wanafunzi na wafanyakazi wa kada zisizo za afya.

Baadhi ya wanachama wa Dar es Salaam’s British Legion Tanganyika Club wakipata maelezo kuhusu uzalishaji wa PPE kutoka kwa Prof. Lawrence Museru.


Na Sophia Mtakasimba

Wanachama na marafiki wa Dar es Salaam’s British Legion Tanganyika Club wametoa msaada wa TZS. 5,425,000 Mil. kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuongeza nguvu kwenye kiwanda cha kuzalisha mavazi ya kujikinga na maambukizi ya Covid-19.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huyo Mwenyekiti wa klabu hiyo Bw. Godfrey Mramba amesema kuwa wameguswa jinsi ambavyo Hospitali ya Taifa Muhimbili iliweza kukabiliana na changamoto kubwa ya upungufu wa mavazi kinga ambayo yalikua hayapatikani kwa urahisi duniani kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa.

“Tunazitambua jitihada zenu kwa jinsi mlivyoweza kuanza uzalishaji kutoka vazi kinga 120 hadi 600 kwa siku sawa na ongezeko la 400% ya uzalishaji hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa vazi hilo,” alisema Bw. Mramba. 

 Amesema kutokana na hilo wanachama na marafiki wa Dar es Salaam’s British Legion Tanganyika Club kwa pamoja waliona watoe mchango wao kuwezesha kiwanda hicho kuendelea kuzalisha bidhaa zinazohitajika kuhudumia Watanzania ili kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na janga la Covid 19.

“Kwa namna ya pekee, sisi kama klabu kuna mwanachama mwenzetu mmoja aliugua na akafariki kutokana na ugonjwa huu. Pia baadhi ya wanachama wengine wameugua wamepona na sasa wanaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida,” amesema Bw. Mramba.

Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru ameishukuru klabu hiyo kuthamini mchango wa hospitali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kusema kuwa kiasi hicho cha fedha kitasaidia ununuzi wa malighafi za kushona mahitaji ya watoa huduma wa hospitali.

“Muhimbili ndio ilikuwa ya kwanza kuzalisha vazi kinga hili nchini baada ya upatikanaji wake kuwa adimu duniani ambapo hadi hivi sasa tumefanikiwa kuzalisha PPE zaidi ya 14,553 kati ya hizo 5,000 zimesambazwa MSD na nyingine katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya, taasisi zisizo za kiserikali, hospitali binafsi, makampuni, Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini,” amesema Prof. Museru

 Katika hatua nyingine, Prof. Museru amesema tayari kiwanda kimeanza kufanya uzalishaji wa barakoa za nguo ili zitumike kwa jamii kubwa ya wanafunzi wa Muhimbili ambao wanategemea kufungua vyuo wiki ijayo pamoja na wafanyakazi wa kada zisizo za afya.