Bodi ya Wadhamini Muhimbili yatembelea miradi zaidi ya Shs. bilioni 9.7

Injinia Salha Mgomba wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akifafanua jambo kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuhusu teknolojia ya juu ambayo mashini mpya ya MRI inatumia kutoa huduma za uchunguzi kwa wagonjwa.

Pichani ni mashini mpya MRI ambayo imefungwa hivi karibuni Muhimbili.

Daktari Bingwa wa Mgonjwa ya Watoto wa Muhimbili, Dkt. Edna Majaliwa akifafanua jambo wakati wajumbe wa bodi walipotembelea miradi ya hospitali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru akifafanua jambo kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya hospitali wakati walipoitembelea wodi namba mbili ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum.

Kiongozi wa wodi ya kinamama wanaohitaji uangalizi maalum katika Jengo la Wazazi Muhimbili, Bi. Alice Msonde akifafanua jambo kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya Muhimbili.


Na John Stephen

Bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ya hospitali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 9.7.

Miradi ambayo imekaguliwa na bodi ni wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (PICU), wodi za watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalumu (NICU), wodi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma ya matibabu ya figo, wodi namba moja na mbili ambako wanalazwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na idara inayosimamia vipimo mbalimbali vya hospitali.

Katika ziara hii, Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Chalers Majinge aliutaka uongozi wa Muhimbili kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya kwa lengo la kuwafikia wagonjwa wengi zaidi.

“Kwa kweli uongozi wa Muhimbili umefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma, tunawapongeza kwa kazi walizoifanya na wanazoendelea kufanya,” amesema Prof. Majinge.

Amesema ubunifu uliofanywa na Muhimbili ndio unaimarisha utoaji wa huduma bora za ubingwa wa juu sambamba na juhudi za wataalam wabobezi.

Naye Mkurugenzi wa Muhimbili akizungumzia ufungaji wa mashini mpya ya MRI amesema italeta tija kubwa na kutoa huduma za ubora wa hali ya juu kwa kuwa ina teknolojia ya kisasa.

Amefafanua kwamba faida kubwa ya mashini hiyo itasaidia kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wengi kwa muda mfupi na kuchunguza kwa undani  magonjwa mbalimbali kupitia kwa wataalam.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa bodi, Bw. Isaya Mwita Charles  baada ya kutembelea miradi amesema uboreshaji wa huduma unaofanywa na hospitali una  manufaa makubwa kwa wananchi pamoja na wataalam. 

Katika ziara hii, mwenyekiti na wajumbe walishuhudia wataalam wabobezi wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa mbalimbali waliolazwa Muhimbili.