Australia Tanzania Society Yafadhili Madaktari Muhimbili

Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Shirika Lisilo la Kiserikali Australia Tanzania (ATS), Didier Murcia akizungumza kwenye hafla ya kutoa ufadhili wa masomo ya upasuaji (plastic surgery) kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Madaktari waliopatiwa ufadhili ni; Dkt. Ibrahim Mkoma na Dkt. Edwin Mrema wa hospitali hiyo.

Baadhi ya wageni walioudhuria hafla hiyo wakimsikiliza mwenyekiti huyo wakati akieleza jitihada za ATS na Muhimbili za kutoa huduma za upasuaji kwa watu waliopata ajali za moto, ajali za barabarani na wenye tatizo la mdomo sungura.

Dkt. Ibrahim Mkoma wa Muhimbili akipokea vifaa tiba vya upasuaji kutoka kwa mwakilishi wa Australia Tanzania Society (ATS).

Dkt. Baruani akipokea vifaa tiba kwa niaba ya Dkt. Edwin Mrema kutoka kwa mwakilishi wa Australia Tanzania Society (ATS), James Chialo.


Na John Stephen

Shirika Lisilo la Kiserikali Australia Tanzania (ATS) limetoa ufadhili kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa upasuaji (plastic Surgery) kwa watu wenye tatizo la mdomo sungura pamoja na wale waliopata ajali za barabarani na ajali za moto.

Lengo la kutoa ufadhili kwa Dkt. Ibrahim Mkoma na Dkt. Edwin Mrema  kusoma katika  chuo chochote duniani ni kuwajengea uwezo wa kufanya upasuaji kwa watu waliopata ajali za moto na wenye tatizo la mdomo sungura.

Mbali na ATS kutoa ufadhili huo shirika hilo kupitia Rafiki Surgical Missions na Muhimbili wamekuwa wakishirikiana kutoa elimu na kufanya upasuaji kwa watu wenye matatizo hayo nchini.

Mwenyekiti wa shirika hilo Didier Murcia amesema kuwa tangu mwaka 2004, Rafiki Surgical Missions imekuwa ikituma wataalamu kutoka Australia kwa ajili ya kubadilisha maisha ya watu kwa wale wenye tatizo la mdomo sungura na waliopata ajali.

“Kila mwaka wataalamu wetu wanakuja Tanzania kwa ajili ya kutoa huduma kwa watu waliopata ajali na hadi sasa zaidi ya watu 2,500 wamefanyiwa upasuaji wakiwamo watoto na watu wazima,” amesema Murcia.

Murcia amesema kwamba Watanzania wengi wamenufaika kupitia huduma za upasuaji na hivyo watu waliozaliwa wakiwa na tatizo la mdomo sungura na waliopata ajali-baada ya upasuaji wamekuwa wakirejea katika hali zao za kawaida.

“Mpango huu unanufaisha familia, jamii na Tanzania kwa ujumla. Lakini nipende kuwashauri wazazi kwamba watoto wanaozaliwa na tatizo la mdomo sungura wanatakiwa kufanyiwa upasuaji mapema ili kurejesha sura ya mtoto katika hali ya kawaida, watoto wasiachwe hadi wanakuwa watu wazima,” amesema Murcia.

Naye Dkt. Mkoma alishukuru ATS kwa kuwapatia ufadhili wa kwenda kusoma nje ya nchi na kwamba masomo hayo yatasaidia kuwaongezea utaalamu ambao watautumia kufanya upasuaji kwa watu mwenye matatizo hayo.

“Udhamini huu utasaidia kuongeza utaalamu katika upasuaji kwa watu wenye tatizo la mdomo sungura pamoja na wale walipata ajali ya moto,” amesema Dkt. Mkoma.