127 Wapatiwa mafunzo kwa njia ya vitendo Mloganzila

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza na madaktari pamoja na wauguzi tarajali, kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Njoikiki Mapunda.

Madaktari na wauguzi tarajali wakimsikiliza Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dkt.Julieth Magandi.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt Julieth Magandi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madaktari na wauguzi tarajali waliohitimu mafunzo yao.


Na Neema Wilson Mwangomo & Lightness Mndeme

Madaktari na wauguzi tarajali 127 wamehitimu mafunzo kwa njia ya vitendo yaliyolenga kuwapatia uzoefu wa kutoa huduma bora za afya kulingana na taaluma zao.


Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ambayo ni nadharia na vitendo yalikuwa yakitolewa katika  Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila huku yakizingatia vigezo vilivyowekwa na Baraza la Ukunga na Uuguzi Tanzania (TNMC) na Baraza la Madaktari Tanzania (MAT).


Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji MNH, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amewataka wahitimu hao kuwa mfano mzuri katika kutoa huduma bora za afya.


“Tunaamini mtakuwa mabalozi wazuri katika kutoa huduma bora za afya kwa jamii kama ambazo zinatolewa na hospitali yetu” amesema Dkt. Magandi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi, Redemptha Matindi amewashauri wahitimu hao kujenga tabia ya kufanya kazi kwa pamoja katika maeneo watakayopangiwa kwani utoaji huduma za afya huhitaji ushirikiano mzuri kati ya watoa huduma.