Muhimbili yaiwezesha Hospitali ya Amana mashine za milioni 306

Hii ni moja ya mashine ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo iliyofungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana ambayo thamani yake ni TZS. 70 mil.

Mashine ya kusaidia mgonjwa kupumua ambayo itafungwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana ina thamani TZS. 56 Mil.

Mtambo wa kuchuja maji (Portable RO System) kwenda kwenye mashine ya kusafisha damu una thamani ya TZS. 28 Mil. na tayari umefungwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana.


Na John Stephen

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefunga mashine tatu za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo zenye thamani ya TZS. 210 Mil. na inatarajia kufunga mashine moja ya kusaidia mgonjwa kupumua (ventilator) yenye thamani ya TZS. 56 Mil. katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ili kuhudumia wagonjwa waliopata maambukizi ya virusi vya CORONA.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa MNH, Bw. Aminiel Aligaesha amesema wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa damu, tayari wameanza kuhudumiwa na wafanyakazi wa MNH waliopo Hospitali ya Amana tangu Ijumaa ya tarehe 24 Aprili, 2020 saa 12 asubuhi.

Sambamba na hilo, Hospitali imefunga mtambo wa kuchuja maji (Portable RO) wenye thamani ya TZS. 28 Mil na mtandao wenye miundombinu ya kusafirisha maji ili kuwezesha mashine hizo kufanya kazi ya kusafisha damu uliogharimu TZS. 12 Mil.

Bw. Aligaesha amesema jumla ya gharama ya mashine hizo TZS. 306 Mil. na kwamba dawa na vitendanishi vya kutoa huduma ya kusafisha figo hivi sasa vinagharamiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Aidha, MNH kupitia Hospitali ya Upanga na Mloganzila, ilipokea wagonjwa 93 kutoka Amana wakiwemo watoto wachanga 30 chini ya mwezi mmoja wakiwa na mama zao, watoto wanne chini ya miaka mitano, kina mama wajawazito 36, wagonjwa wa upasuaji 10 na wagonjwa 13 wenye magonjwa ya ndani (internal medicine).

“MNH vile vile itapokea madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Amana kuanzia tarehe 28 Aprili, 2020 ili kuwajengea uwezo wataalamu wa Kitengo cha Kusafisha Damu pamoja na vyumba tofauti vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICUs),”amesisitiza Bw. Aligaesha. 

Amesema, MNH imekua bega kwa bega na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye maandalizi ya kupokea wagonjwa waliopata maambukizi ya Corona katika Hospitali Rufaa ya Amana ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wagonjwa waliolazwa wanapata huduma. 

Mbali na hayo, MNH inatoa rai kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na kuwakinga wengine ili wasipate maambukizi ya virusi vya Corona kama Serikali inavyoelekeza.