EMAT yatoa mafunzo ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi nchini

Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Elias Kwesi akizungumza kwenye Kongamano la kisayansi lililofanyika tarehe 1 mpaka 3 Oktoba 2019.

Baadhi ya wataalam wakifanya mafunzo kwa njia ya vitendo. Mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Dar es Salaam.

Baadhi ya wataalam wa afya wakishiriki mafunzo hayo.

Wataalam wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kongamano la kisayansi lililofanyika tarehe 1 mpaka 3 Oktoba 2019.


Na John Stephen

Chama wataalamu wa Tiba ya Dharura na Ajali Nchini Tanzania (EMAT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imeendesha mafunzo ya tiba ya dharura ya kuokoa maisha ya wagonjwa wenye dharura za afya, ajali na mahututi  kwa wataalamu wa afya  zaidi ya 180 katika mikoa na wilaya mbalimbali hapa nchini.

Kwa mujibu wa Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe, mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika kampasi ya MUHAS Dar es Salaam na yalihusisha watoa huduma zaidi ya 180 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

 Lengo kuu la mafunzo kwa njia ya vitendo ambayo yalitolewa kuanzia tarehe 1 mpaka 3 Oktoba 2019 ni kuwawezesha watoa huduma nchini kuwa tayari kutoa huduma za kuokoa maisha kwa kutumia mbinu mbalimbali za kitaalamu.

 “EMAT imejiwekea malengo ya kuhakikisha kuwa, kwa kushirikiana Wizara ya Afya na wadau wengine inatimiza lengo la kuwa na huduma bora za tiba ya dharura kwa Watanzania wote, hivyo mafunzo haya ni hatua muhimu sana ya kutimiza malengo hayo”, amefafanua Dkt. Sawe.

Naye Katibu wa EMAT ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili MNH), Dkt. Juma Mfinanga amesema kuwapo kwa wataalamu wabobezi wa kutoa huduma za dharura na ajali, kumesaidia kuboresha huduma MNH na kupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia 45.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo, Dkt. Kilalo Mjema amesema washiriki walifundishwa jinsi kutumia vifaa vichache wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura. 

“Kama unataka kumpima mgonjwa mapigo ya moyo na hakuna mashine, daktari au muuguzi anapaswa kutumia njia mbadala ili kuokoa maisha ya mgonjwa,”amesema Dkt. Kilalo.

Mratibu wa mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Irene Kulola amesema washiriki wote walipata mafunzo stahiki ili kuokoa maisha ya kila Mtanzania nchini. 

Mafunzo hayo yalihitimishwa  na kongamano kuu la kisayasi “3rd Tanzanian Conference on Emergency Medicine’ na mgeni rasmi katika kongamano hilo  alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainabu Chaula.

Mkutano huo wa watoa Huduma za Tiba ya Dharura na Ajali nchini umehudhuriwa na wataalamu zaidi ya 200 kutoka mikoa na wilaya mbalimbali nchini.