Dkt. Gwajima awataka wananchi kuzingatia taratibu wakati wa kuchukua miili ya marehemu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wataalamu wa afya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuhusu uboreshaji wa huduma za afya. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru na kulia ni Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi, Dkt. Praxeda Ogweyo.

Baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa kwenye kikao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru akifafanua jambo kwa Waziri wa Afya.

Wataalamu wakifuatilia taarifa za kikao hicho.

Mtaalamu wa Patholojia, Prof. Amos Mwakigonja wa Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS) akiwa katika kikao hicho.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja, Bw. Aminiel Aligaesha akifafanua jambo kuhusu uboreshaji wa huduma za afya.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Muhimbili, Muhiddin Mahmoud akieleza jinsi huduma za matibabu ya magonjwa ya figo zinavyotolewa kwa wagonjwa.

Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima akiwasalimia wataalamu wa afya Muhimbili.

Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima akitoa ufafanuzi kuhusu huduma ya kuchukua miili katika Hospitali ya Muhimbili.

Prof. Museru na Dkt. Gwajima wakielekea katika ukumbi wa mikutano kuzungumza na wataalamu wa afya.


Na John Stephen

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi kufuata mifumo na taratibu za kuchukua miili ya marehemu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuondokana na malalamiko kwamba hospitali imekuwa ikizuia kuichukua kwa ajili ya kwenda kuihifadhi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipofanya ziara katika hospitali hiyo kuangalia utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu alilolitoa baada ya kuapishwa mapema mwaka huu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hospitali zisizuie miili ya marehemu. 

Dkt. Gwajima amewataka wananchi kufuata taratibu za kuchukua miili ya marehemu kwa mfano kuwa na vielelezo vinavyotakiwa kwani wengi wamekuwa wakienda vyumba vya kuifadhi miili bila kuwa na vielelezo. 

Amesema kero na malalamiko ambayo amekuwa akipelekewa yanatokana na wananchi au ndugu wa wagonjwa kutofuata mifumo na taratibu za kuchukua miili ya marehemu kwenye vyumba vya kuiifadhi.

“Nimegundua ndugu wa marehemu wanatoka wodini na kwenda katika vyumba vya kuhifadhi miili bila kuwa na vielelezo vya kutosha, nawaomba ndugu kutoa ushirikiano kwa wahusika ili miili ichukuliwe kwa wakati,” amefafanua Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima.

Katika ziara hiyo pia ameagiza uongozi wa hospitali kushughulikia kero haraka ili ndugu wa wagonjwa waendelee na shughuli za maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri ameagiza uongozi wa hospitali kufuatilia ndugu wa wagonjwa wenye uwezo wa kulipia matibabu, lakini wamekuwa wakienda  kwa viongozi wa Serikali za mitaa kupatiwa barua ili kutibiwa bure, huku wakijua kwamba haki hiyo inawahusu bali ni kwa wale waziojiweza tu.

“Ukifuatilia katikati ya mifumo yetu, utabaini matapeli wameingilia mifumo na wanaohudumiwa si walengwa. Sasa ninaiagiza hospitali kufanya uchunguzi wa barua zilizoletwa hapa Muhimbili na tukibaini barua hizo ni za kugushi, fedha zote zilizotumika kuwahudumia wagonjwa ambao si wa msamaha, wahusika watapaswa kulipa fedha zote,” amesema Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima.