This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. +255 222151367/9

Staff EmailFacebook Google Plus Red Cap

 

News and Announcements 

 

EMAT, Muhimbili Wapongezwa Kwa Kutekeleza Mikakati ya Serikali

Dar es Salaam - 13/10/2017

Serikali imekipongeza Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kuendelea kutekeleza mpango wa Serikali wa kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi nchini.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi kutoka hospitali za mikoani na wilayani ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa mahututi na ajali.

EMAT, MNH, MUHAS pamoja na wadau mbalimbali ilianza kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi kutoka hospitali mbalimbali nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa kuhakikisha inaokoa maisha ya wagonjwa wa dharura na ajali kupitia wataalamu wa Afya waliopo mikoani na wilayani.

Akifungua Mkutano wa EMAT, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kwa kuwa dharura hutokea mahali popote na kwa kila mtu ni muhimu sababu mpango huo umekuwa ukiokoa maisha ya wagonjwa kwa zaidi asilimia 45.

“Najivunia kuona kazi kubwa inayofanywa na EMAT ambayo inasaidia kutekeleza mpango wa Serikali wa kusambaza huduma za dharura hapa nchini. Serikali inatambua juhudi zenu na tunawahakikishia tutaendelea kuwaunga mkono ili muendelee kuboresha huduma za dharura nchini,” alisema Dkt. Mpoki.

Katibu Mkuu amesema ili kuhakikisha wagonjwa mahututi wanaendelea kuokolewa, Serikali imewasomesha wataalamu bingwa wa magonjwa ya dharura na ajali 27 ambao wanafanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini.

Amesema Serikali itaendelea kuwasomesha wataalamu zaidi wa huduma ya dharura na ajali ili kuhakikisha kila mkoa unakuwa wataalamu bingwa wa huma hiyo.

“Sasa hivi tutafungua idara ya magonjwa ya dharura na ajali katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Mkoa ya Maount Meru Arusha na baadaye kwenda katika hospitali za mikoa na wilaya nchini,” amesema.

Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe amesema chama hicho kimejiwekea malengo kwa kushirikiana Wizara ya Afya na wadau wengine ili kutimiza lengo la kuwa na huduma bora za tiba ya dharura kwa Watanzania wote.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Dkt. Upendo George amesema EMAT ikishirikiana na MNH, MUHAS, Abbot Fund Tanzania Stanbic Bank, MSD, Dkt. Ntuyabaliwe Foundation, Aga Khan na MOKAS imetoa mafunzo ya siku mbili kwa washiriki zaidi ya 150 kutoka hospitali mbalimbali nchini ili kuwawezesha kutumia vifaa vichache vilivyopo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Irene Kulola amesema washiriki wote kutoka sehemu mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo stahiki ili waweze kuwafundisha wenzao jinsi ya kuokoa maisha kwa wagonjwa wa dharura na ajali.

Naye Katibu wa EMAT ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga amesema kuwapo kwa wataalamu waliobobea katika kutoa huduma za dharura na ajali katika hospitali hiyo kumesaidia kuboresha huduma na kupunguza vifo.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika mkutano wa Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) ambao umefanyika jijini Dar es Salaam leo.

Baadhi ya washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi wakiwa kwenye mkutano huo leo.

Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe akieleza juhudi zilizofanywa na chama hicho katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa magonjwa ya dharura na ajali nchini.

Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Rais wa EMAT leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Mpango Endelevu wa Abbot Foundation, Dkt. Festo Kayandabila akiueleza mkutano huo jinsi mfuko huo unavyoshirikiana na EMAT katika kutoa mafunzo kwa wataalamu wa magonjwa ya dharura na ajali nchini.

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki.

 

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

EMAT Yaanza Mafunzo ya Kuokoa Maisha ya Wagonjwa Mahututi Nchini

Dar es Salaam - 12/10/2017

Chama cha Watoa Huduma za Magonjwa ya Dharura Tanzania (EMAT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wameanza kutoa mafunzo kwa vitendo jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura kwa wataalamu mbalimbali wa afya.

Lengo la mafunzo hayo ni kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya dharura na ajali nchini kwani utoaji bora wa huduma ya magonjwa ya dharura na ajali imesaidia kupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia 45 duniani.

Kwa mujibu wa Rais wa EMAT, Dkt. Hendry Sawe, mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika kampasi za Muhimbili, MUHAS na Hospitali ya Aga Khan na kwamba yanahusisha watoa huduma zaidi ya 150 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Dkt. Sawe amesema lengo la kuu la mafunzo kwa njia ya vitendo ambayo yameanza kutolewa leo hadi kesho ni kuwawezesha watoa huduma nchini kuwa tayari kutoa huduma za kuokoa maisha kwa kutumia mbinu mbalimbali za kitaalamu kwenye hospitali zao.

“EMAT kwa kushirikiana Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine, tunatimiza lengo la kuwa na huduma bora za tiba ya dharura kwa Watanzania wote, hivyo mafunzo haya ni hatua muhimu sana ya kutimiza malengo hayo,” amesema Dkt. Sawe.

Rais huyo amesema mafunzo hayo pamoja na mkutano yanaratibiwa na EMAT kwa kushirikiana na MHN, MUHAS, Aga Khan, MSD, Abbot Fund Tanzania, Stanbic Bank, MOKAS na Dkt. Ntuyabaliwe Foundation.

Naye Katibu wa EMAT ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Juma Mfinanga amesema kuwapo kwa wataalamu waliobobea katika kutoa huduma za dharura na ajali, kumesaidia kuboresha huduma katika hospitali hiyo na kupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia tano.

Katika hatua nyingine, Dkt. Pendo George ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo amesema washiriki wanafundishwa jinsi ya kutumia vifaa vichache vilivyopo wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.

“Kama unataka kumpima mgonjwa mapigo ya moyo na kukuna mashine, daktari au muuguzi anapaswa kutumia njia mbadala ili kuokoa maisha ya mgonjwa,”amesema Dkt. Pendo.

Mratibu wa mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Irene Kulola amesema washiriki wote watapata mafunzo stahiki ili kuokoa maisha ya kila mtanzania nchini. Amesema washiriki kutoka mikoa mbalimbali na nchi za jirani wamehudhuria mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa na kongamano kuu la kisayasi ‘Tanzanian Conference on Emergency Medicine’ ambalo litafanyika Ijumaa wiki hii tarehe 13/10/2017 kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. Mgeni Rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dkt. Kilalo Mjema wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akitoa mafunzo jinsi ya kuokoa maisha ya mtoto mdogo kwa washiriki mbalimbali.

Washiriki mbalimbali wakimsikiliza Dkt. Ramadhani Juma wa hospitali hiyo wakati akitoa mafunzo ya vifaa gani vinapaswa kutumika kwa mgonjwa mwenye tatizo la kupumua.

Muuguzi Songoma John wa Muhimbili akiwaeleza washiriki jinsi kumpatia huduma mtoto mwenye tatizo katika mfumo wa njia ya hewa (choking)

Baadhi ya washiriki wakijifunza mafunzo ya uongozi katika kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa.

Dkt. George Dilunga akitoa mafunzo kwa washiriki jinsi ya kumuhudumia mgonjwa mwenye tatizo la kupumua (respiratory failure).

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Muhimbili Yapewa Msaada wa Thamani Sh10 Milioni NMB

Dar es Salaam - 06/10/2017

Kaimu Mkurugenzi wa Uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zuhura Mawona ameishukuru Benki ya NMB kwa kuipatia hospitali hiyo msaada wa wenye thamani ya Sh 10 milioni.

Benki hiyo imetoa magodoro 35, vitanda vitatu na mashuka 100 ikiwa ni utaratibu wa kurejesha faida kwa wateja wa benki hiyo.

“Msaada huu utatumika kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania wengi, hivyo tunaomba muendelee kuisaidia Muhimbili kwani inahitaji msaada zaidi,” amesema Zuhura.

Naye Meneja wa NMB tawi la Muhimbili, Lukas Malua amesema benki hiyo imetenga Sh 1 bilioni ikiwa ni sehemu ya faida yake ili kurejesha faida hiyo kwa jamii.

Meneja wa NMB tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Lukas Malua akikabidhi msaada wenye thamani ya Sh 10 milioni kwa Kaimu Mkurugezi wa Uuguzi wa hospitali hiyo, Zuhura Mawona. Msaada uliokabidhiwa leo ni magodoro 35, mashuka 100 na vitanda vitatu.

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Serikali Yaipongeza Muhimbili kwa Kutoa Huduma Bora

Dar es Salaam.

Serikali imepongeza juhudi zinazofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) za kuboresha huduma sanjari na kuwawezesha watalaam kusoma ili wapate ujuzi zaidi na kutoa huduma bora na za kibingwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulusubisya wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo kupitia Idara ya Usingizi.

Dk. Mpoki amesema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na uongozi wa hospitali na kwamba hatua hiyo inaleta faraja kwa Watanzania kwani sasa wana uhakika wa kupata huduma bora .

“Naona mabadiliko makubwa hapa Muhimbili, mmeongeza vyumba vya upasuaji, Vyumba vya wagonjwa mahutuni (ICU) na pia mnaendelea kuboresha huduma zingine kwakweli hatua hii ni ya kupongezwa na ninaomba muendelee kujituma kwani hospitali hii inategemewa kwa sababu mna watalaam wengi waliobobea hapa,’’ amesema Dk. Mpoki.

Kuhusu kusomesha wataalam, Katibu Mkuu amesema hatua hiyo ni nzuri kwani watalaam hao watapata fursa ya kuwatawafundisha wengine ili nao wapate ujuzi .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru amesema MNH inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa wataalam katika Idara ya Usingizi na kwamba hospitali inaendelea kutatua changamoto hizo.

Dk. Mpoki ambaye ameambatana na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dk. Doroth Gwajima pamoja na mambo mengine wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwemo vyumba vya upasuaji, wodi ya wagonjwa mahututi na wodi ya watoto.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulusubisya (kulia) akitembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo ili kuona maeneo mbalimbali yaliokarabatiwa vikiwamo vyumba vya upasuaji na vyumba vya kulaza wagonjwa wa figo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulusubisya akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Uzingizi leo pamoja na watumishi wengine wa hospitali hiyo

Baadhi ya wafanyakazi wa idara hiyo pamoja na watumishi wengine mbalimbali wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Ulusubisya leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Ulusubisya kuzungumza na wafanyakazi wa idara hiyo leo.

Wafanyakazi wa Muhimbili wakiwamo wa Idara ya Usingizi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Museru.

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Muhimbili Yazindua Mwongozo wa Kuwahudumia Watoto Wachanga

Na John Stephen

Dar es Salaam, Tanzania. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imezindua muongozo utakaosaidia kuwahudumia watoto wachanga( Neonatal Guideline) wenye umri kuanzia siku 0 hadi siku 28 ili kuhakikisha wanapata huduma inayostahiki.

Muongozo huo umeandaliwa na madaktari wa MNH na kupitiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na Chuo Kikuu cha Kwazulu Natal kilichopo Afrika Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru amesema muongozo huo si tu unamanufaa kwa MNH bali pia una manufaa kwa hospitali zingine kwani utawezesha mtoto kupata tiba inayotakiwa hata sehemu ambazo hakuna watalaam.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto Edna Majaliwa ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wachanga wa hospitali hiyo amesema kuwepo kwa muongozo huo kutasaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga sanjari na kupunguza rufaa za watoto hao kuletwa Muhimbili .

‘’ Kusudio letu ni kuendelea kupunguza vifo vya watoto wachanga , MNH tumefanikiwa kupunguza vifo hivyo kutoka 26 kwa kila vizazi hai 1,000 na kufikia 18 kwa kila vizazi hai 1,000. Kwa mwaka watoto wanaozaliwa hapa ni takribani 10,000 hivyo naamini muongozo huuu utaleta mabadiliko makubwa‘’ amesema Dk. Majaliwa.

Pia ameelezea vyanzo vinavyosababisha vifo vya watoto wachanga kuwa ni madhara ya kuwa njiti, mtoto ambaye amezaliwa na hakulia pamoja na mtoto mwenye vimelea vya bakteria.

Akiwasilisha mada kuhusu muongozo huo , Daktari wa watoto , Jullieth Cosmas ametaja sababu zinazochangia watoto wachanga kulazwa Hospitalini kuwa ni mtoto kuzaliwa kabla ya wakati(Njiti) mtoto kushindwa kupumua vizuri pindi anapozaliwa , mtoto kupata maambukizi , mtoto kutolia wakapi alipozaliwa na mtoto kuumia wakati akizaliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza katika uzinduzi wa kitabu chenye mwongozo jinsi ya kutoa huduma ya afya kwa watoto wachanga wenye umri sufuri hadi siku 28. Uzinduzi huo umefanyika leo katika hospitali hiyo.

Daktari wa watoto wa hospitali hiyo, Dk. Judith Cosmas ambaye ameshiriki kuaanda kitabu hicho akizungumza kwenye mkutano huo.

Baadhi ya wataalamu wa afya wakiwa kwenye mkutano huo leo.

Mkuu wa Idara ya Watoto, Dk. Merry Charles akisisitiza jambo huku akionyesha kitabu hicho ambacho kitakuwa kikitumika wakati wa kuwahudumia watoto hao.

Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Museru (kaunda suti) akiwa kwenye mkutano huo leo.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya MNH na wadau mbalimbali.

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Cuba Yaipongeza Muhimbili Leo kwa Kutoa Huduma Bora

Na John Stephen

Balozi wa CUBA nchini ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo na kuipongeza hospitali hiyo kwa kutoa huduma nzuri za afya.

Ujumbe kutoka ubalozi huo umetembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma, ikiwamo vyumba vya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), vyumba vya upasuaji na maeneo mengine ya kutoa huduma.

Hospitali hiyo inashirikiana na Cuba katika kutoa huduma ya afya na imeahidi kuendelea kushirikiana na MNH kwa ajili ya kuboresha huduma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema hospitali hiyo itaendelea kushirikiana na Cuba ambayo imeahidi kupeleka wataalamu wake katika hospitali hiyo.

“Tunaushukuru ubalozi wa Cuba kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha, hii ni moja ya njia nzuri ya kutekeleza malengo yetu,” amesema Profesa Museru.

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo ameipongeza Muhimbili kwa kufanya upanuzi mkubwa katika majengo mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma bora.

“Nimefurahishwa na huduma bora, pia vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalimu ni vizuri na vimekizi mahitaji ya wagonjwa,” amesema Balozi Polledo.

Naye Mkurugenzi wa Upasuaji, Dk Julieth Magandi amesema Cuba imekubali kuipatia Muhimbili wauguzi waliobobea katika kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.

“Cuba imekubali kuipatia Muhimbili madaktari wawili waliobobea katika kutoa huduma za uzingizi, madaktari bingwa wawili wa kutoa huduma katika vyumba vya upasuaji na daktari bingwa mmoja wa mionzi,” amesema Dk Magandi.

PICHA NA JOHN STEPHEN, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo akizungumza na baadhi ya wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakati akiitembelea leo. Kushoto ni Mratibu wa madaktari wa Cuba nchini, Dk Maylen Lopez. Kutoka kushoto wa tatu ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Muhimbili, Makwaia Makani, Mkurugenzi wa Upasuaji, Dk. Julieth Magandi, ofisa Idara ya ufundi, Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Hedwiga Swai, Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru na Mkurugenzi wa Ufundi, Gaudence Aksante.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na Balozi wa Cuba nchini, Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo. Kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi, Gaudence Aksante.

Balozi wa Cuba nchini, Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Museru leo kabla ya kutembelea maeneo ya kutoa huduma katika hospitali hiyo.

Balozi wa Cuba na baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo wakiwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU)

Ujumbe kutoka Ubalozi wa Cuba ukiwa katika chumba cha upasuaji Muhimbili leo.

Baadhi ya wakurugenzi wa Muhimbili wakiwa katika picha ya pamoja na ubalozi wa Cuba leo baada ya kuitembelea hospitali hiyo.

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Wizara ya Afya Malawi Yatembelea Muhimbili , Waipongeza Kwa Kutoa Huduma Bora

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imepokea ujumbe wa wataalamu wa Afya kutoka Wizara ya Afya ya nchini Malawi.

Ujumbe huo umeongozwa na Katibu wa Afya nchini humo , Dk. Dan Namarika umehusisha Madaktari , viongozi pamoja na wataalam mbalimbali kutoka katika Wizara hiyo pamoja na taasisi nyingine za afya .

Akizungumza baada ya kupokea ujumbe huo , Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru amesema ujio wa watalaamu hao unatoa fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Juliethi Magandi amesema katika mwaka wa Fedha 2016-2017 Hospitali imehudumia wagonjwa wa nje Laki Nne , Thelathini na Sita Elfu na Miatatu Tisini na Nne wakati wagonjwa wa ndani waliohudumiwa ni Hamsini na Tisa Elfu na Miatano Hamsini na Tano.

Akizungumzia lengo la ujio wao , Katibu wa Afya wa nchi hiyo Dk. Dan Namarika amesema wamekuja kujifunza jinsi ambavyo MNH inafanya kazi na kutekeleza mipango yake .

Lengo la serikali ya Malawi na Wizara ya Afya kwa ujumla ni kuhakikisha inaboresha utoaji wa huduma hususani katika Hospitali za Umma nchini humo.

Ujumbe usema kuwa umefurahishwa jinsi Muhimbili inavyotoa huduma za kibingwa na kusomesha wataalamu wa afya nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa mafunzo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na ujumbe kutoka Malawi ambao umetembelea hospitali hiyo LEO ili kujifunza jinsi inavyoboresha huduma za afya. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchini Malawi, Dk. Dan Namarika.

Ujumbe kutoka Malawi wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Museru.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Muhimbili, Dk Julieth Magandi akieleza muundo wa hospitali kwa ujumbe wa Malawi.

Wakurugenzi wa Muhimbili wakiwamo watalaamu wengine wa afya wakimsikiliza Dk Magandi leo.

Ujumbe wa Malawi ikiongozwa na wenyeji wao wakiwa katika Jengo la Watoto leo.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali (EMD), Dk Juma Mfinga akitoa ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa na idara hiyo.

Ujumbe kutoka Malawi ukiwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

 

 

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Muhimbili Yazindua Mfumo wa Kulipia Huduma za Afya kwa Kadi Maalumu

31/08/2017

Na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imezindua mfumo wa kulipia huduma za afya kwa kutumia kadi maalumu.

Huduma hiyo tayari imeanza kutolewa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na Kampuni Maxcom Afrika ambayo imepokelewa vizuri na wagonjwa pamoja na dugu wa wagonjwa.

Lengo la kulipia huduma za afya kwa kutumia mfumo huo ni kupunguza muda mwingi ambao wagonjwa wamekuwa wakitumia wakati wa kupatiwa huduma hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema MNH imekamilisha awamu ya kwanza ya usimikaji wa mfumo wa malipo kwa njia ya kielekroniki kwa kutumia kadi maalumu ya malipo au kwa kutumia simu za mkononi.

“Awamu ya pili wagonjwa au ndugu wa wagonjwa wataanza kulipia huduma za afya kupitia kadi zao za benki aina ya viza au Mastercard. Pia, hospitali itaongeza wigo wa kulipia kwa njia ya simu za mkononi kwa kupitia mitandao ya TTCL Pesa, Halopesa na Easypesa,” amesema Profesa Museru.

Malipo kwa njia ya Kadi Maalumu (Muhimbili Card)

  1. Mgonjwa au jamaa wa mgonjwa atapewa Kadi Maalumu na Wakala wa Muhimbili (Maxcom) ambapo atatakiwa kuijaza fedha.
  2. Baada ya kujaza fedha kwenye Kadi, mgonjwa ataelekea eneo la kutolea huduma na atapewa Hati ya Gharama (Bill Note) na kutakiwa kulipa. Atatumia Kadi yake kwa kuigusisha katika mashine ndogo (POS) na mashine hiyo itakata kiasi kilichooneshwa katika Hati ya Gharama na kutoa risiti ya mashine.
  3. Mgonjwa ataendelea kutumia Kadi yake kulipia gharama na endapo fedha kwenye Kadi zitakwisha atarudi kwenye dirisha la Wakala na kujaza tena fedha. Ikiwa fedha zitabaki kwenye Kadi Mgonjwa atakuwa na hiari ya kuziacha kwenye Kadi kama akiba au kuomba arejeshewe fedha taslimu.

Malipo kwa MPESA, TIGOPESA na Airtel Money

Wakati Mgonjwa atakapopewa Hati ya Gharama (Bill Note) na akiamua kuchagua kulipia kwa kutumia simu yake atafuata utaratibu ufuatao:

  1. Kwa mfano MPESA, mteja ataanza kwa kubonjeza
    *150*00#;
  2. Baada ya hapo atachagua huduma namba 4 ‘’LIPA kwa M-Pesa’’;
  3. Baada ya hapo atachagua huduma namba 4 ‘’Weka namba ya Kampuni ‘’, ambapo mgonjwa atajaza namba 356666 ambayo ni namba ya Hospitali ya Taifa Muhimbili;
  4. Baada ya hapo mgonjwa atatakiwa kuweka namba ya kumbukumbu ya malipo. Hapa mgonjwa atajaza namba iliyopo kwenye Hati ya Gharama (Bill Note) ambayo ni ‘’Mobile Request Number’’;
  5. Mgonjwa atapata ujumbe kupitia simu yake ikimtaarifu kuwa muamala wake umekamilika na fedha zimetumwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kwa mitandao yote ya simu mgonjwa atafuata taratibu zote hapo juu baada ya kubonyeza *150*01# kwa mteja wa Tigopesa na *150*60# kwa mteja wa AirtelMoney.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Maxcom Africa,Jameson Kasati akimkabidhi KADI ya MALIPO Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru. Kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Gerald Jeremiah wa hospitali hiyo. Kadi hiyo itatumika kulipia huduma za afya katika hospitali hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari Leo kuhusu mfumo wa kulipia huduma za afya kwa kutumia kadi maalamu. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Maxcom Africa,Jameson Kasati na kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Gerald Jeremiah.

Baadhi ya maofisa wa Muhimbili na Maxcom Africa wakifuatilia mkutano huo Leo ambao umefanyika katika hospitali hiyo. Wengine waliokaa nyuma ni waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo leo.

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Gerald Jeremiah wa Muhimbili akitoa maelezo jinsi ya kulipia huduma za afya kwa kutumia KADI ya Malipo ambayo imetengenezwa MNH kwa kushirikiana na Muhimbili.

Baadhi ya maofisa wa Muhimbili wakifuatilia mkutano huo leo.

Ofisa Masoko wa Kampuni ya Maxcom Afrika, Deogratius Lazari akiwaeleza waandishi wa habari jinsi wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanavyolipia huduma za afya kwa kutumia kadi maalimu.

 

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

MTOTO ALIYEUNGUA MIKONO SASA KUREJEA DARASANI

18/08/2017

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Mtoto Mwanahidi Hamisi akiwa na mama yake, Amina Mohamed Mkadengile katika Hospitali ya Taifa Muhimbili

Mtoto aliyeungua na kushindwa kuendelea na masomo mkoani Mtwara ametibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na sasa anaweza kuendelea na masomo pamoja na kufanya shughuli zake za kawaida.

Mtoto huyo aliungua moto baada ya kusukumwa na mwenzake shuleni na hivyo kuungua mikono yote miwili na kusababisha vidole kujikunja na kushikamana.

Baada ya kufikishwa Muhimbili madaktari bingwa walifanyia upasuaji na sasa amepona.

Daktari Bingwa wa Upasuaji, Ibrahimu Mkoma amesema mtoto Mwanahidi Hamisi aliungua miaka saba iliyopita na mikono yake kuadhirika na kushindwa kufanya kazi yoyote.

Amesema mwaka 2015 mtoto huyo alifanyiwa upasuaji mkono wake wa kulia katika Hospitali ya CCBRT na kwamba sasa anaendelea vizuri.

Dk Mkoma amesema Juni 7, 2017 Muhimbili ilimpokea mtoto huyo na baada ya kufanyia uchunguzi walimfanyia upasuaji mkono wa kushoto na kunyoosha viungo katika vidole vyake ambavyo vilikuwa vimejikunja.

“Baada ya kuungua moto vidole vyake vilishikana na viungo kujikunja, lakini tumefanikiwa kuvinyoosha viungo hivyo na sasa Mwanahidi anaendelea vizuri na matibabu,” amesema Dk Mkoma.

Amesema mtoto huyo sasa anaweza kufanya kazi mbalimbali kama kufua na kwamba anaweza kundelea na shule tofauti na awali baada ya kuungua.

Mama wa mtoto huyo, Amina Mohamed Mkadengile ameambiwa kwamba anapaswa kumfanyia mazoezi mtoto wake ili aimarike zaidi.

“Daktari amenielekeza jinsi ya kumfanyia mtoto mazoezi, nitakuwa nafanyia mazoezi katika Hospitali ya Mkoa ya Ligula mkoani Mtwara. Nawashukuru sana madaktari wa Muhimbili na wauguzi kwa kunipatia huduma nzuri,” amesema mama wa mtoto huyo.

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Taasisi ya SUKOS yakabidhi vifaa vya Zimamoto Hospitali ya Muhimbili

28/07/2017

Taasisi ya Maafa, Majanga na Uokoaji -SUKOS, leo ameikabidhi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) vifaa vya zimamoto ili kusaidia uokozi mara yanapotokea majanga ya moto.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Suleiman Kova amesema wameamua kutoa msaada huo katika hospitali hiyo kwa kuwa imekuwa ikitoa huduma nzuri za afya.

“Tulifanya utafiti tukavutiwa na huduma nzuri zinazotolewa Muhimbili hivyo tumeanza na Muhimbili na baadaye tutaenda kutoa msaada kwenye taasisi nyingine. Kama mnavyojua tunafanya kazi ya kijitolea,” amesema Kova.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru ameshukuru Muhimbili kupatiwa msaada huo na kwamba vimetolewa wakati muhafaka.

Mkurugenzi wa Ufundi, Gaudence Aksante amesema vifaa hivyo vitatunzwa ili viweze kutoa huduma iliyokusudiwa.

Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)

Mkurugenzi wa Taasisi ya Maafa, Majanga na Uokoaji -SUKOS, Suleiman Kova (kulia) akimkabidhi vifaa vya zima moto Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru kwa ajili ya kutoa huduma ya uokoaji endapo itatokea majanga ya moto katika maeneo ya kazi au majumbani. Kulia ni Mkurugenzi wa Ufundi, Gaudence Aksante.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru akishukuru baada ya kupokea msaada huo Leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Suleiman Kova na Mkurugenzi wa Ufundi, Gaudence Aksante akifuatilia tukio hilo.

Meneja wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Astrade Tanzania, Abdallah Massawe akielezea matumizi ya kifaa maalumu cha kutoa taarifa mara gesi inapokuwa ikivuja kwenye mtungi. Kifaa hicho kinasaidia watumiaji wa gesi kuchukua taadhari mara gesi inapoanza kuvuja.

Mmoja wa wafanyakazi wa Taasisi ya Maafa, Majanga na Uokoaji –SUKOS, Ramadhani KHamisi akionyesha jinsi ya kuzima moto baada ya kutokea mlipuko sehemu za kazi au majumbani.

 

Maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Damu Duniani Yafana Muhimbili

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imeshiriki katika madhimisho ya Siku ya Kuchangia Damu duniani kwa kuendesha shughuli ya utoaji damu kwa watu mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa wagonjwa wenye uhitaji.

Shughuli hiyo inaendelea katika hospitali hiyo kwenye Jengo la Maabara kuu ambako watu wamekusanyika kwa ajili ya kuchangia damu. Mmoja wa viongozi walishriki katika maadhimisho hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Sophia Mjema pamoja na Watanzania mbalimbali.

Akizungumza katika shughuli hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo wakiwamo kinamama na watoto wadogo.

“Nawapongeza wote walifika leo hapa Hospitali ya Muhimbili kuchangia damu, ni jambo la muhimu mmefanya kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa,” amesema Mheshimiwa Mjema.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi wa hospitali hiyo, Dk Praxeda Ogweyo amewataka wananchi,mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali, shule, vyuo mbalimbali na taasisi za dini kujitokeza kuchangia damu hospitali hapo.

Dk Ogweyo amesema kuwa Muhimbili inahitaji wastani wa chupa za damu 100 hadi 120 kwa siku na kwamba damu inayokusanywa ni kati ya chupa 50 hadi 60 na upungufu wa damu ni chupa 60 hadi hadi 70, hivyo damu inahitajika zaidi.

“Kutokana na hali hii, naomba rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuokoa maisha ya wagonjwa. Hospitali imejipanga kupitia kitengo chake cha uchangiaji damu kilichopo maabara kuu hivyo karibuni mchangie damu,” amesema Dk Ogweyo.

PICHA NA JOHN STEPHEN, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Sophia Njema akizungumza na Jonas Hans Atile (kushoto) ambaye amejitokeza kuchangia Damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Leo.

 

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Praxeda Ogweyo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kuchangia Damu Duniani. Pia Dk. Ogweyo amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kuchangia damu.

 

Mmoja wa Wananchi akishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Uchangiaji Damu duniani Leo katika hospitali hiyo.

 

Baadhi ya wananchi wakisubiri kuchangia damu Leo katika jengo la Maabara kuu, hospitali ya Taifa Muhimbili.

 

Baadhi ya Wananchi waliojitokeza kuchangia damu katika Hospitali ya Muhimbili wakiendelea na shughuli ya utoaji damu Leo.

 

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------- 

 

MWILI WA MZEE FRANCIS MAIGE KANYASU ‘NGOSHA’ WASAFIRISHWA MWANZA LEO

Mwili wa marehemu Mzee Francis Maige Kanyasu umeagwa leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kusafirishwa na serikali kwenda kijijini kwao Igokero wilayani Misungwi.

Shughuli ya kuuaga mwili huo imeongozwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamaii , Jinsia , Wazee na Watoto, Marcel Katemba ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Mpoki Ulusubisya.

Akizungumza katika shughuli hiyo Bwana Katemba ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa jitihada kubwa walizofanya za kumpatia tiba na kumuhudumia kwa kipindi alichokuwa amelazwa hospitalini hapo.

“Nawapongeza Muhimbili kwa juhudi zenu ni kweli mlitaka kuokoa maisha ya mzee wetu, lakini kazi ya Mungu haina makosa , pia sina budi kuwashukuru majirani zake na uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Malapa kwa kujitoa naomba mfanye hivyo hata kwa wazee wengine’’ amesema Katemba.

Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dk. Juma Mfinanga amesema walimpokea Mzee Kanyasu Mei 25, 2017 akitokea Hospitali ya Amana alikokua akipatiwa matibabu na walipomfanyia vipimo vya awali waligundua kwamba ana maradhI ya Kifua Kikuu ambayo alikuwa nayo kwa muda mrefu kutokana na mazingira aliyokua akiishi.

Hivyo Dk. Juma ametoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kwenda hospitalini mapema pindi mtu anapoona hali yake ya kiafya si nzuri kwani ukiwahi hospitali ni rahisi kupata tiba na kupona kuliko kusubiri hadi ugonjwa uwe sugu.

Mzee Francis Maige Kanyasu alizaliwa 1931 na kufariki dunia Mei 29 , 2017 saa mbili na nusu usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

 

Baadhi ya wawakilishi kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakiaga mwili wa marehemu Francis Maige Kanyasu (86) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo. Marehemu alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo na wakati akiendelea na matibabu mauti yakamkuta.

 

Mwili wa marehemu ukiwa umebebwa tayari kwa safari ya kuelekea Misungwi mkoani Mwanza ambako mazishi yatafanyika.

 

Baadhi ya wafanyakazi wa Muhimbili wakisubiri kuuaga mwili huo leo. Kulia ni Zuhura Mawona ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Uuguzi, Agness Mtawa na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk Julieth Magandi.

 

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Marcel Katemba ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulusubisya akizungumza kabla ya shughuli za kuaga mwili huo leo.

 

Baadhi ya watu waliofika kuaga mwili huo leo.

 

Mkurugenzi wa Huduma na Upasuaji wa Muhimbili, Dk Julieth Magandi akiwashukuru watu mbalimbali walofika kuuaga mwili huo leo.

 

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali wa Muhimbili, Dk Juma Mfinanga akieleza jinsi Hospitali ya Muhimbili ilivyokuwa ikimpatia matibabu mzee Francis Maige Kanyasu.

Other Menu
Useful Links
Polls
How do you rate our site?
Visitor Counter

Today 109

Yesterday 178

This Week 287

This Month 3207

All 33819

Kubik-Rubik Joomla! Extensions